Watu mil. 1.24 hufa kwa ajali za barabarani duniani kila mwaka.



Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohammed Mpinga
Takriban watu milioni 1.24 hupoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na ajali za barabarani.
 
Hayo yalisemwa na Dk. Elias Kwesi, kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto wakati wa warsha ya uzinduzi wa kazi za ufuatiliaji wa masuala ya usalama barabarani kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
 
"Jamii kutokuwa na elimu juu ya masuala ya usalama wa barabarani hali hiyo imesababisha watu kila mwaka kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu,'' alisema.
 
Dk. Kwesi aliongeza kuwa hospitali nyingi zina majeruhi wengi wa ajali ambao wengi wao ni vijana, hali inayochangia taifa kupoteza nguvu kazi.
 
Alisema ajali za barabarani zinasababisha serikali kutumia mamilioni ya fedha, pia damu kutumika kwa wingi kuwaongezea majeruhi.
 
Dk. Kwesi alisema ili ajali ziache kutokea na kulitia taifa hasara, inatakiwa watu wafuate sheria na kanuni za usalama barabarani ikiwamo na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nao kupewa elimu.
 
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafirishaji hawapendi kuviboresha vyombo vyao na badala yake hujali maslahi, hali ambayo husababisha ajali kutokea kutokana na vyombo kutokuwa na ubora unaotakiwa.
 
Mgeni rasmi katika warsha hiyo, Ofisa Mnadhimu wa Kikosi cha Usalama Barabani Makao Makuu, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Fortunatus Muslim, alisema inatakiwa kazi zifanywe kwa pamoja ili kusaidia kupunguza ajali  za barabarani.
 
Muslim alisema pia sheria zinatakiwa kufanyiwa mabadiliko hali itakayosaidia kupunguza ajali za barabarani.
 
Alifafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2015, ajali zilitokea zilikuwa 8,383 na kusababisha vifo 3,468 na majeruhi 9,383.
 
Aidha, Muslim alisema takwimu zinatakiwa kutumika ili kuwajengea uelewa wananchi wajua ukweli wa ajali pale zinapotokea na siyo kupotosha.
 
Alisema masuala ya usalama hayapewi kipaumbele wakati watu wanakufa huku wengine wakipata ulemavu.
 
"Taasisi nyingi zinaanzishwa, lakini hakuna hata moja ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya barabarani, hivyo inatakiwa kuliangalia hilo ili kufanikisha kupunguza ajali na siyo kuliachia Jeshi la Polisi pekee kukabiliana na masuala ya barabarani,'' alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment