FAMILIA katika nyumba saba zilizopo mtaa wa Mageuzi, kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga zimekumbwa na hofu baada ya kudai kukuta kitu kama damu katika milango yao, huku familia moja ikipewa vitisho vya kuchomewa nyumba kwa kudaiwa Sh milion 11.
Familia hizo zilikuta dumu lenye ujazo wa lita tano likiwa na mafuta ya petroli na ujumbe wa vitisho ukiandikwa kwa maandishi mekundu katika kitambaa cheupe. Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Emmanuel Joshua aliyekuwa eneo la tukio alisema uongozi wa mtaa kwa kushirikiana na Polisi na wananchi wa mtaa huo, wanaendelea kufanya uchunguzi wa matukio hayo na watachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.
“Haya matukio yamewatia hofu wakazi wa eneo hili, tunaomba wananchi wasiyahusishe na imani za kishirikina kwani pengine kuna watu walifanya uhalifu na kupita maeneo ya familia hizi wakiwa wanavuja damu, tunaomba tushirikiane kuwafichua wahusika wa matukio haya”, alisema.
Alikiri kuwa familia zimekuta kitu kama damu na ujumbe wa vitisho kuwa familia moja nyumba yao itachomwa moto na kwamba wanawatafuta watu waliofanya tukio hilo lililozua taharuki kwa watu hao.
Wahusika wa tukio hilo, Lucas Massaba na Hosea Himo kwa nyakati tofauti walisema tukio la kumwagwa damu kwenye milango yao linaashiria dalili mbaya hivyo kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutolipuuza na kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo.
Massaba alisema familia yake imeingiwa hofu kwani haijulikani watu walioweka vitu hivyo na vitisho wana lengo gani na alisisitiza lisipuuzwe na vyombo vya usalama. Mmiliki wa nyumba iliyotishiwa kuchomwa, Hamis Reli Mathayo na mke wake Loyce Busumba, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, walikuta dumu lenye lita tano likiwa na petroli na kitambaa cheupe, vyote vikiwa na maandishi mekundu ya vitisho kuwa watachomewa nyumba yao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Dismas Kisusi alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi aliyekuwepo eneo la tukio, alisema bado hajapokea taarifa kuhusu matukio hayo.

0 comments:
Post a Comment