
Baada ya mchezo wa jana kati ya Simba dhidi ya Azam, kocha msaidizi wa Simba Adam Abdallah amekiri kwamba Yanga inaelekea kuwa bingwa kutokana na wao kuchemka kupata ushindi kwenye mchezo wao dhidi ya Azam mchezo ambao ungewasogeza kwa poini 5 nyuma ya Yanga.
Licha ya kukiri kwamba Yanga inanafasi kubwa ya kutwaa taji la VPL msimu huu, Abdallah amesema bado hawajakata tamaa na wataendelea kupigana hadi mwisho kwani lolote linaweza kutokea.
“Mchezo dhidi ya Azam ulikuwa muhimu sana kushinda kutokana na matokeo yetu ya nyuma ya kupoteza mechi mbili kwahiyo tulitaka kurudisha imani kwenye mbio zetu za ubingwa, lakini mchezo wa mpira kama ulivyo unamatokeo matatu na tunamshukuru Mungu hatujapoteza mchezo”, anasema Adam Juma ambaye ameisimamia Simba tangu Mayanja alipopewa adhabu ya kuondoka kwenye benchi la ufundi wakati wa mchezo dhidi ya Toto Africans.
“Tumepambana tukapata nafasi tatu za kufunga lakini tumeshindwa kuzitumia, narudia tena, lolote linawezekana muhimu kwetu ni kupambana mwanzo hadi mwisho baada ya hapo tutajua nani anakuwa bingwa”.
“Hadi sasa Yanga ndiyo inaongoza na inaonekana kuwa na muelekeo wa ubingwa lakini na sisi tunapambana mpaka mwisho kujua hatma yetu”.
Zikiwa zimesalia mechi nne kati ya timu tatu zinazo wania taji la VPL, Yanga ndiyo wanaongoza ligi wakiwa na pointi 65 wakifuatiwa na Azam wenye pointi 59 na Simba wakishika nafasi ya tatu kwa pointi zao 58.

0 comments:
Post a Comment