Kocha
wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Mjerumani, Martine Grelics,
amesema kuwa yupo tayari kuchukua jukumu la kuinoa Simba kwa msimu ujao
na ikafanya vizuri.
Mjerumani
huyo ambaye aliondoka katikati ya msimu uliomalizika hivi karibuni, kwa
sasa yupo nyumbani kwao akifanya kazi ya kuwanoa wachezaji mbalimbali
kwenye kituo chake cha soka cha Alpenkick Fussballschule.
Simba
ambayo mwanzoni mwa mwaka huu ilimtimua kocha wao, Muingereza, Dylan
Kerr na mikoba yake kuchukuliwa na Mganda, Jackson Mayanja, kwa sasa ipo
kwenye mchakato wa kumleta kocha mwingine atakayesaidiana na Mayanja.
Licha
ya majina ya makocha wanaotakiwa na Simba bado hayajawekwa hadharani,
lakini jina la Muingereza, Boby Williamson aliyewahi kuinoa timu ya
taifa ya Uganda, limekuwa likitajwa mara kwa mara kuchukua mikoba hiyo.
Grelics
akiwa kwao Ujerumani, amesema tangu alipoondoka amekuwa akiendelea
kulifuatilia soka la Tanzania na baada ya kuona msimu wa ligi
umemalizika, akaona ni bora kuanza kusaka timu ya kuifundisha hapa Bongo
na kuona Simba inahitaji kocha, hivyo yupo tayari kuifundisha.
“Nipo
kwenye mchakato wa kurudi tena Tanzania kufundisha soka kwani maisha
niliyoishi awali nilipokuwa na Toto Africans, nilibaini kwamba
Watanzania ni wakarimu sana.
“Kwa sasa naangalia ni jinsi gani naweza kutuma CV zangu kwenye Klabu ya Simba, endapo nitapata jukumu la kuinoa Simba, wala wasiwe na wasiwasi kwani kwa uwezo nilionao naamini nitaipa mafanikio makubwa Simba,” alisema Grelics


0 comments:
Post a Comment