Na Saleh Ally
INAWEZEKANA kabisa bila ya ubishi ni mateso makubwa kuwa shabiki wa timu ya Simba kwa kipindi hiki.
Mashabiki
wa Simba wanaumia kwa kuwa hawana kile wanachokitaka, wanakitafuta
lakini hawajakipata na kabla ya kukipata, wengine wamekipata na
wanaendelea kukipata.
Huu
ni msimu wa nne sasa, Simba haijashiriki michuano ya kimataifa. Lazima
ukumbuke Simba ni timu yenye sifa hiyo, kushiriki na kufanya vizuri nje
ya Tanzania.
Rekodi
zinaibeba kwenye mambo mengi sana. Timu ambayo imefanya vizuri zaidi
kwa ukanda wa Afrika Mashariki katika michuano ya ukanda huo kwa kuwa
wamechukua mara nyingi zaidi.
Bado
rekodi zinaibeba Simba Afrika. Ndiyo timu pekee ya Tanzania kufikia
fainali ya michuano mikubwa zaidi kwa upande wa klabu. Hii ni kwa Afrika
Mashariki yote, wao ndiyo pekee wamecheza fainali ya Kombe la Caf mwaka
2003.
Kwa
miaka hii minne, miwili wakati wa uongozi wa Ismail Aden Rage na miwili
chini ya Evans Aveva, Simba imefeli na imewafanya baadhi ya Wanasimba
kuona kwamba mambo sasa yameshindikana.
Miaka
minne bila ya mafanikio hata kidogo. Awali ilionekana Simba imeteleza
tu, msimu wa pili ikaonekana itajirekebisha. Wa tatu, utakuwa wa mwisho
na sasa ni wanne, mwisho wa haya utakuwa baada ya muda gani?
Aveva
aliichukua Simba kwa Rage ikiwa imechoka kwa misimu miwili mfululizo.
Mategemeo ilikuwa ni kurekebisha, sasa ni misimu miwili tena, mambo ni
yaleyale.
Huenda
huu ni wakati mzuri Wanasimba wakaanza kutafakari na kupata majibu
ambayo yatakuwa sahihi kwa ajili ya wao kubadili gia. Kweli wamefeli
misimu minne bila ya mafanikio hata kidogo.
Hata
iwe vipi, lazima tukubali, Simba kufeli kwa misimu minne si jambo dogo
hata kidogo. Simba si Ndanda wa JKT, kila mmoja anaujua ukubwa wake kama
ambavyo nilianza kuelezea.
Kama
kweli vipindi vizuri vimeyeyuka na vile vigumu vimeendelea mfululizo
huku vikiendelea kutanua mioyo ya Wanasimba kwa maumivu. Wao ndiyo
watakuwa waamuzi wazuri wa njia sahihi ya kupita.
Inawezekana
kabisa wakafanya maamuzi ya hasira au kukomoana, ukawa ni wakati wa
kujiangusha pia kutengeneza njia nyingine ya kuendelea kuumia kwa miaka
mingine nane. Ikiwezekana ikafikia siku na kusema: “Huu ni mwaka wa
nane, Simba bado haijabeba kombe wala kushiriki kimataifa”.
Wakati
kunapokuwa na tatizo, inawezekana mkafanya uamuzi fulani ambao lazima
muupime na kujua utakuwa unaleta matokeo ya kuharibu zaidi au kusaidia.
Umakini wa juu unahitajika hapa.
Ushauri
wangu, uongozi wa Simba ufikie wakati sasa ukubali kila ulipokosea na
kuanza kurekebisha, lakini kuna kila sababu ya kukutana na wanachama
ndani ya siku kadhaa baada ya ligi kwisha.
Wanachama
ndiyo wenye timu, wapewe nafasi ya kutoa dukuduku. Uongozi upokee na
kukaa kuangalia yaliyo sahihi, uyafanyie kazi kwa manufaa ya klabu hiyo.
Baada ya hapo waanze tena, mwisho watachanganya.
Lakini
kwa wale wanaotaka uongozi kwa udi na uvumba, basi wanapaswa kukumbuka
maana ya maslahi ya Simba. Tamaa yao ya madaraka isiiangushe Simba kwa
miaka mingine minne. Wafikirie kwamba kuiangusha kabisa, ni kujitwika
mzigo baadaye hata wakipata nafasi ya kuiongoza.
Hakuna
asiyejua, viongozi wakitaka madaraka, basi huangalia maslahi yao kwa
maana ya kutaka kushinda hata kama wanaanzisha kitu ambacho kitaanzisha
chuki au kuporomoka kwa jambo muhimu la klabu.
Huu
ni wakati mzuri wa kuangalia maslahi ya klabu yenu kwanza. Vizuri
muungane na kushirikiana, baada ya hapo mengine yatafuatia.
Hakika,
kama Simba iendelee hivi tena, basi wa kulaumiwa watakuwa Wanasimba
wenyewe, kuanzia viongozi, makocha, wachezaji lakini hata wanachama.
Hapa ninatia msisitizo, wakati huu ni wa kuelezana ukweli, kuwa na moyo
wa kweli wa mapenzi ya klabu na sahauni ubinafsi. Mliokosea mkubali
kuelezwa na kurekebisha, msipofuata haya, mtavuruga zaidi ya hapa.

0 comments:
Post a Comment