YANGA ITAENDA KATIKA UCHAGUZI, ILA SI KWA SHINIKIZO, IACHWE ICHEZE MPIRA


Na Baraka Mbolembole
Yanga SC hawana sababu ya ‘kuchanganyikiwa’, kamati ya uchaguzi TFF inapeleka utengano? Mara zote kwenye mchezo wa soka kuna presha, na pengine timu ya Yanga SC inakwenda kupitia kipindi chake chenye presha ndani na nje ya uwanja.
Kamati ya uchaguzi ya Shirikisho la soka nchini ( TFF) imetoa ‘tamko la amri’ kuutaka uongozi wa klabu hiyo chini ya mwenyekiti wake Yusuph Manji kuitisha mkutano mkuu wa uchaguzi mapema Juni. Kila mtu anafahamu kuhusu harakati za uchaguzi jinsi zinavyokuwa zikiwagawa watu. Lakini mbona TFF inawalazimisha watu wasio tayari na jambo hilo?
Siku chache baada ya kamati ya uchaguzi ya TFF, wakili Aloys Komba kuitangazia Yanga tarehe ya kufanya uchaguzi wao, wazee wa klabu hiyo walipiga hodi hadi ofisi za baraza la michezo la Taifa (BMT), walikwenda na ujumbe kwamba ‘hawataki kufanya uchaguzi na wangependa timu yao iachwe icheze mpira!’
Kuna kitu kibaya wamekiona kinaweza kutokea wakati huu klabu yao ikipigania taji la ligi kuu, huku wakihitaji matokeo mazuri katika dakika 180 tu kabla ya kuweka rekodi ya timu ya kwanza ukanda wa Afrika Mashariki kufuzu kwa hatua ya makundi ya michuano ya Shirikisho Afrika.
Muda wa Manji kuwa madarakani kama mwenyekiti wa klabu ulikwishamalizika tangu katikati ya mwaka 2014. Ikumbukwe, Manji aliingia madarakani katikati ya mwaka 2012 baada ya kushinda uchaguzi wa dharura kufuatia kujiuzulu kwa ‘shinikizo la wanachamana’ kwa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu tangu mwaka 2010, wakili Lyod Nchanga.
Wakati wa mkutano wa mwaka wa klabu mwaka 2014 huku wakitambua kuwa ni mwaka wa uchaguzi, asilimia zaidi ya 98 wanachama hawakutaka kuona Manji anaicha klabu yao ndiyo maana walifikia hatua ya kumuomba Manji kuendelea kuiongoza timu yao hata kwa miaka nane zaidi! Jambo ambalo Manji mwenyewe alilikataa na kusema siyo ‘msingi wa demokrasia.’
Baada ya kuombwa sana, huku baadhi ya wanachamana wakilia na kutoa machozi, Manji akatoa pendekezo la kumpatia mwaka mmoja zaidi kisha klabu iitishe mkutano mkuu wa uchaguzi na si kukaa madarakani kwa miaka nane au sita bila kufanyika kwa uchaguzi.
Wanachama wakakubaliana na Manji akaongoza klabu yao bila kuwapo kwa kelele za ndani ya klabu-kwamba amevunja katiba ya klabu. Hata TFF ilijaribu kupingana na hilo lakini hawakubadilisha chochote. Mwaka ukakata, lakini sasa ni zaidi ya miezi 20 na Manji hakuwa amesema lolote kuhusu uchaguzi wa klabu. Wanachama pia wamekaa kimya, timu inacheza mpira.
Ni nadra sana kuona hali ya utulivu katika timu ya Yanga kama kiongozi amemaliza muda wake, lakini Manji ameweza ndiyo maana nimekuwa nikisema mtu huyu ( Manji) ni kati ya viongozi makini ambao Yanga wamepata kuwa naye.
Unaweza kukataa au kukubali lakini ukiyapima matendo yanayotendeka ndani ya Yanga hivi sasa na kulinganisha na miaka ya nyuma hadi nyakati za Nchunga ni wazi ameweza kuweka ushawishi mkubwa kwa wanachama ambao wanaamini utawala wake unaweza kuwapa matokeo makubwa siku za mbeleni.
Jiulize ni nani anayekataa Yanga isifanye uchaguzi? Si Manji bali ni wapiga kura na wagombea ambao TFF inawalazimisha waende kufanya mabadiliko na kufuata katiba yao inayowaongoza ambayo imekiukwa karibia mwaka wa pili huu.
Wanachama wa Yanga wana hofu ya kumpoteza Manji kwa kudhani kwamba hatochukua fomu na kugombea kwa muhula mwingine baada ya kipindi chake cha mpito kumalizika.
Hofu ya wanachama kumpoteza Manji wakati huu timu yao ikikabiliwa na ushindani mwingine mkali kutoka klabu za Azam FC na Simba SC ndiyo inayopeperusha chaguzi za klabu hiyo kwa maana wanachama wanaamini bila Manji wanaweza kuingia katika kipindi kigumu kama nyakati za Nchunga.
Manji ameipa Yanga taji moja la VPL na miaka yake mitatu katika michuano ya CAF timu imefika 16 bora mara mbili. Hakika wana Yanga wanakwenda katika presha lakini maamuzi ni yao wenyewe na wanaweza kushusha presha yao kama tu watakwenda na ushawishi mzuri na kumuomba Manji agombee tena.
Ni lazima Yanga iende katika uchaguzi ila si muhimu ufanyike katika tarehe waliyopanga kamati ya uchaguzi ya TFF. Kama walivyotaka wazee wa klabu hiyo kwamba timu yao iachwe icheze mpira kwanza wakati huu, nami naunga mkono, Yanga iachwe icheze mpira lakini ni lazima pia iende katika uchaguzi.
Inawezekana kitendo cha kuanza kwa mchakato wa uchaguzi kinaweza kuleta makundi tofauti klabuni na kama hilo litatokea itakuwa ni hatari sana kwa Yanga.
Kamati ya uchaguzi ya TFF ni kama inapeleka utengano klabuni hapo katika wakati ambao watu wameshikamana ila wako sahihi na wamefanya kazi yao kuwakumbusha Yanga kuhusu kufanya uchaguzi lakini si kuwapangia kwa shinikizo.
Manji atagombea tena Yanga kwa maana ana ndoto kubwa za kuisaidia klabu hiyo na hajapata kuzitimiza hadi sasa. Anaipenda klabu na wanachama wanamkubali hivyo hakuna sababu ya wana Yanga kuingia katika presha wakati imani yao kiutawala iko kwa mtu mmoja tu.
Njia pekee ya Yanga kuepuka presha ya nje ya uwanja wakati huu ni kutozungumzia mambo ya uchaguzi katika vyombo vya habari zaidi maendeleo ya timu yao ndani ya uwanja.
Yanga waende tu katika uchaguzi na wakamshawishi tena Manji agombee kiti alichokalia sasa. Yanga SC itaenda katika uchaguzi, ila si kwa shinikizo, iachwe icheze mpira’.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment