VITA YA MADRID: DAUDI NA GOLIATI WANAPOZALIWA NDANI YA TUMBO MOJA!

Real-Madrid-vs-Atletico-Madrid
Real-Madrid-vs-Atletico-Madrid
Mwanaume ni kiumbe aliyeumbwa na ujasiri mkubwa wa kuzidhibiti hisia zake ndani ya mishipa ya moyo wake. Ni rahisi mwanaume kujikausha hasa akiwa na hisia za huzuni na majonzii, lakini tatizo moja lisilokwepeka ni MACHOZI.
Yapata majira ya saa sita kasoro usiku usiku kwa majira ya jiji la Milan, Italia. Baada ya kumalizika pambano la fainali ya UEFA Champions League uwanja mzima unageuka kambi ya maombolezo. Atletico Madrid wamefungwa kwa penalti 5-3 na majirani zao wa Real Madrid, wachezaji na makocha wa Atletico Madrid wanalia sambamba na wafuasi wao ‘Él Colchoneros’, lakini kinachostaajabisha ulimwengu ni unapoona mashabiki na wachezaji wa Real Madrid wakipandisha jezi nyeupe kuzificha nyuso zao zenye machozi.
Wote wanajua Dunia na maisha havitendi haki, Madrid wametumia zaidi ya Euro Million 800€ kukusanya wachezaji bora popote ulimwenguni na kuwekwa chini ya mtaalamu Zinedine Yazid Zidane ‘Zizou’ lakini bado nafsi zinaumia wanapoyatazama mateso ya majirani zao wa Atletico. Florentino Perez anatambua wazi Dunia haina usawa lakini afanyaje zaidi ya kuondoa miwani machoni mwake ajipanguse machozi usoni?
Ilipoanzia Vita Ya Wenyewe Kwa Wenyewe
Real Madrid na Atlético Madrid ni vilabu vinavyopishana umaarufu, mafanikio na utajiri kwa kiasi kikubwa, japokuwa vina thamani sawa ndani historia ya jiji la Madrid. Tofauti na ‘derby’ nyingi tunazozijua kama ya United Vs City jijini Manchester na Inter Vs AC Milan pale Italia, hata Yanga Vs Simba pale Kariakoo, vita ya
Madrid ‘El Derbi madrileño’ imetawaliwa na ubabe wa Real zaidi.
Zikiwa zimeshacheza mara 213 Real wakishinda mara 108 na Atletico mara 54, huku zikishuhudiwa draw 51.
Real Madrid ni watoto wapendwa na nembo ya ufalme na ubwanyenye, wakati Atletico walitambulishwa kama watoto watukutu na waasi.
Hata makao makuu ya vilabu hivi yanasawiri uhalisia wa maisha yao, wakati Santiago Bernabeu ikisimama ‘uzunguni’ mwa jiji mkabala na majengo ya benki na shopping malls mashuhuri za Chamartín, Atletico madrid wamejificha pale Vicente Calderon kusini kabisa mwa mji wakizungukwa na kelele za viwanda vya magodoro na pombe na bugudha nyingine za makazi ya walalahoi.
Pengo Kubwa la Idadi ya Mataji
Licha ya kiu kubwa ya mashabiki wa Atletico kutaka shuhudia timu yao ikiwanyoosha mabishoo wa Real Madrid, lakini mwishoni mwa siku timu yoyote inatambuliwa kwa idadi yake ya mataji.
Hii ni habari nyingine mbaya inayowafanya wainamishwe vichwa chini kadri wanavyohesabu shibe ya vikombe kwa jirani na miayo ya kabati lao la kuhifadhia mataji.
Ligi Kuu Spain/La liga
Real Madrid: 32, Atletico Madrid: 10
Kombe la mfalme/Copa del Rey
Real Madrid: 19, Atletico Madrid: 10
Ngao ya jamii/Copa de Espana
Real Madrid: 9, Atletico Madrid: 2
UEFA Champions League
Real Madrid: 11, Atletico Madrid: 0
UEFA Europa Cup/League
Real Madrid: 2, Atletico Madrid: 2
UEFA Super Cup
Real Madrid: 2, Atletico Madrid: 2
FIFA World Cup/Inter-Continental
Real Madrid: 4, Atletico Madrid: 1
Kwa kipindi hiki itakuwa ni vema kuiangalia derby ya Madrid katika mizani ya kabla na baada ya Diego Simeone kupewa mikoba ya ukocha pale Atletico, msimu wa Krismasi 2011.
  1. a) Kabla ya Ujio wa Diego(2011)
Atletico kilikuwa kituo rasmi cha Real kujikusanyia pointi 3 za kilaini kabisa. Upinzani baina yao haukuwa na afya kabisa, mfano mzuri pale Atletico ilipocheza mechi 25 kwa misimu 14 (1999-2013) bila kupata matokeo chanya mbele ya wapinzani wao. Hakuna mtu aliyekuwa na muda wala wazo juu ya Él derbì Madrileño.
  1. b) Ujio wa Diego Simeone ‘Él Chollo’ na Tumaini la Wanyonge
Simeone ameibua upya ushindani ndani ya la liga na msisimko katika Madrid derby. Ameirejesha Atletico kuwa katika hadhi ya vilabu vinavyowania ufalme wa Hispania na washindani wa ukweli ndani ya UEFA Champions League.
Uwezo wake wa kuchukua wachezaji wanaoonekana wa kawaida na kuwajaza roho ngumu na ujasiri mioyoni mwao unamfanya Simeone awe zaidi ya kocha katika maisha ya walalahoi wa Madrid.
Amebarikiwa jicho la tatu katika kuvumbua maforward wasiokuwa na jina na kuwageuza wawindaji hatari wa nyavu za wapinzani. Sergio Aguero, Diego Forlan, Radamel Falcao, Diego Costa na sasa Antoine Griezman wote wamekuwa lulu machoni mwa vilabu vikubwa wakitoka katika mikono ya Simeone, kisha kwa pamoja kutambua thamani ya nembo ya klabu katika vifua vya jezi zao.
Ndani ya kipindi cha misimu mitatu amekwishanyakua ubingwa wa La Liga na kuipeleka timu katika fainali mbili za 2014 na 2016 ligi ya Mabingwa, bahati mbaya zote wanapoteza mbele ya maadui zao wakuu.
Unyonge wa Atletico kwa sasa unamuumiza kila mmoja hasa wakazi wote wa jiji la Madrid. Ubingwa wa 11 barani Ulaya kwa Real wakati Atletico wakifungwa katika fainali tatu na bila kuwa na kikombe hata kimoja katika kabati lao ni unyonge usiomithilika.
Hakuna furaha kubwa kwa shabiki wa Atletico zaidi ya kuifunga Real Madrid hasa wakati huu ambao wakiwa wamewang’oa mabingwa wa Spain (Barcelona) na mabingwa wa Germany (Bayern Munich), hakika walistahili kombe hili.
Ronaldo anahitaji medali hizi ili atwae Balon d’Or, Florentino Perez alihitaji ubingwa wa 11 ili abakie na urais wa Madrid, mpaka wamasai wa Makiba, Arumeru waliruka kushangilia Juanfran alipokosa penalti ya Atletico lakini wote ndani ya mioyo yao walikuwa wana hisia za dhati kuishuhudia Atletico Madrid wakimaliza unyonge wa miaka 113 barani Ulaya.
Hatimaye, Jumapili captain Sergio Ramos kwa mara nyingine tena aliwaongoza mamia ya maelfu ya mashabiki wa Real Madrid kwenda kulizungusha kombe katika sanamu ya malkia pale katika mnara wa Cibèles, lakini wote hawana nyuso za furaha kabisa wakifiria masahibu ya jirani zao. Wanazungumza kwa upole mkubwa na kukiri shauku yao ya kushuhudia siku moja Daudi akinyanyuka na kuwa na ubavu wa kumwangusha Goliati penye sakafu.
Hasta la Vista!
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment