| ALI KIBA (KUSHOTO) NA DIAMOND |
KAMA
una simu inayoweza kufungua mitandao ya kijamii, basi ukizubaa utakuwa
na bahati ya kushuhudia madudu tu na simu hiyo haitakuwa na faida kwako
hata kidogo.
Mitandaoni
kuna mambo mengi sana yanaendelea na hayana maana hata kidogo ingawa
wanayoyaendeleza huamini wana uwezo mkubwa wa kuzungumza mambo na
wanachosema ni sahihi hasa.
Kwenye
Facebook, Instagram na Whatsapp ndiko jalala la kila asiye na uwezo
kufikiri au kutafakari na kulichambua jambo. Ili mradi kuna uhuru wa
kutoa maoni, basi kila mmoja ‘anatapika’ anachoona ni sawa. Hata vile
vilivyojaa ujinga, viko mitandaoni na huko vina thamani kubwa kwa kuwa
ndani ya mitandao hakuna kipimo cha madudu.
Nimejifunza
mengi na ajabu zaidi, wachangiaji wa mambo mengi wasiojua mambo,
hujirahishia njia ya uchangiajikwa kuporomosha matusi.
Kutukana
tu, ni sehemu ya kuonyesha uwezo mdogo wa upambanuzi wa hoja pia
inathibitisha mchangiaji ubongo wake una njaa ya ufikiri kwa kiasi gani,
lakini hauna uwezo wa kushiba kabla ya kuendelea na kazi yake.
Wiki
iliyopita, wasanii Nasibu Abdul ’Diamond’ na Ali Saleh ‘Ali Kiba’
walikuwa ni kati ya wale waliopata nafasi ya ushiriki wa tuzo za MTV
Mama ambazo zimefanyika nchini Afrika Kusini na wote walipata nafasi ya
kutumbuiza.
Diamond
alitumbuiza na wacheza shoo wake, Kiba akatumbuiza akiwa na Sauti Soul
wa Kenya ambao wamemshirikisha katika wimbo wao wa ‘Unconditionally Bae’.
Nianza
kwa kuwapongeza Diamond, kwamba walifanya kazi nzuri kabisa. Mapungufu
yalikuwepo kwa kila mmoja wao, kama Diamond na sauti kuonekana ni kama
ni mtu anayepumua kwa nguvu lakini Kiba pia hakuwa na muda wa kutosha
baada ya kuimba sehemu ya ubeti wake na kiitikio ambacho kilipunguzwa.
Haikuwa rahisi kuweza kuona ubora wake vizuri lakini hakika, vijana hawa
wa Kitanzania wanastahili pongezi.
Shoo
ya Diamond, ilikuwa bora kuliko nyingine zote usiku huo ukumbini jijini
Johannesburg, Afrika Kusini. Lakini mitandaoni badala ya mjadala bora
wa nani alifanya nini, kipi kilipungua na wapi kiongezwe, matusi ndiyo
yametawala.
Mimi
niliweka video za vipande vya shoo zao kwenye ukurasa wangu wa
Instagram, lengo likiwa ni kuongeza kuwasambaza vijana hao wa Kitanzania
ambao wanaendelea kuleta heshima na wanawapa changamoto wale ambao
hawajafikia huko.
Diamond
na Kiba si wasanii wa kwanza kuleta heshima nchini. Lakini hadi
wamefikia hapo lazima kabla walifikiri kuwa kama fulani, mfano Lady
Jayedee au AY na wengine ambao walikuwa wakifanya vema kimataifa.
Ajabu
kabisa ni kwamba, walio mitandaoni wanajulikana kama Team Kiba na Team
Diamond. Hawa ni watu ambao wako kwa ajili ya kusifia upande mmoja na
kuupaka matope upande mwingine.
Team
Kiba hakuna wanaloona ni zuri la Diamond, Team Diamond kazi yao ni
kuponda tu upande wa Kiba. Kila unachofanya kama mwanadamu kinakuwa na
faida zake, hasara zake pia.
Ukipima,
utaona Team Diamond na Team Kiba wanafanya kazi ya kupoteza muda, mambo
ya kijinga pia ni watu wasiotafakari kwa kuwa wamejivika kaniki na
wanajaribu kuisafisha kwa ‘jiki’ ambalo si jambo sahihi.
Kaniki
inakuwa jinsi ilivyo, kila unapoifua ni lazima ukumbuke rangi yake,
maana huwezi kuibadili kwa kuifua. Si rahisi kuwaongezea au kuwapunguzia
Diamond na Kiba kwa maneno makali au matusi mitandaoni.
Kama
Kiba na Diamond watakuwa wanazipa nguvu hizo timu, basi hata wao
watakuwa hawajui wanalolifanya na hawafuatilii historia ya muziki kwamba
wapambe kama hao Team Kiba na Team Diamond, huko nyuma walikuwa ni
sehemu ya kufa kwa makundi mfano TKM Wanaume na East Coast.
Mashabiki
badala ya kuburudika, wanaishi na chuki, wanaamini kwenye kutukanana na
kukataa kila kizuri cha wanayemuona ni mpinzani. Hakuna wanaofanikiwa
kwa kukataa mazuri ya waliojitahidi.
Anayefanya
vizuri, jifunze kwake. Pia matusi hayajawahi kuingia kwenye historia
yoyote ya mafanikio, badala yake wanaofanya hivyo huonekana ni
mwendawazimu.
Vizuri
kuepuka kugeuza mitandao kuwa maficho ya wajinga na wanaoweza kusema
lolote. Badala yake, kama kweli nyie ni timu kwa ajili ya kuwasaidia
wasanii hao ambao wote ni Watanzania, basi muwe na mijadala bora yenye
lengo ya kujenga, si kila anayetukana ndiyo anaonekana hakuna kama yeye.
Kumbukeni
hata hawa Diamond na Kiba, siku moja watakwisha na wengine watapaa
kwenye nafasi zao, hili halina mjadakla, hivyo mnaweza kuwasaidia
kuendelea kubaki juu kwa muda mrefu kwa mawazo bora, kukubali kazi ya
mwingine na kukosoa kwa mlengo wa uadui na chuki tu! Vipi unaweza kuwa
shabiki wa burudani, halafu ukatumia muda wote kusambaza chuki wakati
lengo namba moja la burudani ni kuburudisha!

0 comments:
Post a Comment